Simba ilimsajili mshambuliaji nyota wa Gor Mahia ya Kenya, Danny Sserunkuma.
Wakati
anakuja nchini, Sserunkuma alikuwa ametoka kuichezea timu yake ya taifa
ya Uganda kuwania kucheza michuano ya Afcon, lakini wakashindwa katika
hatua za mwisho kabisa.
Alikuja
nchini baada ya mapumziko ya takribani wiki mbili, hivyo uzito
uliongezeka, kasi ilipungua na ilionekana hakuwa na mazoezi ya kutosha.
Ilionekana
alisumbuka sana kuendana na kasi ya Simba na hata Ligi Kuu Bara, lakini
alionyesha kuanza kurejea taratibu katika kiwango chake wakati akiwa
Kenya ambako alikuwa mfungaji bora msimu uliopita.
Alifanikiwa
kuifungia Simba mabao muhimu na kufikisha matatu. Alionekana hakuwa
katika kiwango kizuri sana, lakini hakuna ubishi, alitakiwa muda.
Taratibu,
Sserunkuma alianza kuwekwa benchi. Yeye mwenyewe alianza kuonyesha
mgomo na hata baadaye taarifa za kuwa alisema alikuwa akilazimishwa
kufanya mambo ya kishirikina zilizagaa.
Jana
ameonekana akiwa jukwaani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar wakati
Simba ikipambana na Ruvu Shooting na kushinda kwa mabao 3-0.
Siwezi
kukubaliana na wanaosema Sserunkuma ni garasa. Amekuwa mfungaji bora
zaidi ya mara moja, amecheza timu ya taifa ya Uganda yenye wachezaji
wengi mahiri lakini amepata nafasi.
Inawezekana
anashindwa kuwa bora, huenda ana tatizo, na uongozi au benchi la ufundi
linaweza kuzungumza naye kuhusiana na nini asaidiwe.
Lakini
kama ameshindwa kabisa, huenda ana bahati mbaya na Simba. Basi aachiwe
aende kwa kuwa Simba haiwezi kuwa inaendelea kumlipa zaidi ya dola 1000
(zaidi ya Sh milioni 2.) huku yeye akiendelea kukaa benchi au jukwaani.Hakuna cha kupoteza, Simba inapaswa ifanye uamuzi mgumu ikiwezekana kumuacha mapema ili isiendelee kuingia hasara.Simba
imekuwa ikihaha kupambana na ukata, sasa si sahihi kuendelea kubaki na
mchezaji wa kimataifa anayekaa benchi na kulipwa mshahara bure.Viongozi wa Simba wanapaswa kuwa wachumi, kusaidia pia kuepusha fedha kupotea bila sababu ya msingi.