Uongozi wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Azam FC, umefunguka juu ya mbinu za chinichini zinazoendeshwa na Yanga kuwinda saini ya nyota wao, Didier Kavumbagu kwa kusema kuwa hawawezi kupata kitu.

Kwa muda mrefu Yanga wamekuwa kwenye mpango wa kumrejesha straika huyo Mrundi kwa kile kinachosemekana kuwa ni matakwa ya kocha Mholanzi, Hans van Der Pluijm.

Kavumbagu alisaini mwaka mmoja Azam akitokea Yanga, lakini Azam wakiongea kwa kujiamini wamewaruhusu Yanga kufanya mazungumzo naye kama wanadhani ni mchezaji huru.
Jeuri hiyo imetolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, akisema kuwa wakimgusa kitakachowatokea wasilaumiane.
“(Anacheka), ujue kipindi kama hiki ni kibaya, kila timu inatafuta njia yake. Yanga nia yao ni kutaka kutuondoa kwenye mchezo kwa sababu hatujakutana.

“Lakini pia wao kama wanajiamini wakijua ni mchezaji huru, sisi tunawaruhusu waongee naye halafu waone matokeo yake,” alisema mkurugenzi huyo wa zamani wa mashindano TFF.


Aidha, hakuwa tayari kuweka bayana kama wamemuongezea mkataba, licha ya tetesi zilizoanza kuzagaa kuwa ameongeza miaka miwili.

Advertisement

 
Top