IMG_4759

Kwanza nianze kwa kuwapongeza Yanga s.c kwa kazi waliyoifanya katika mechi dhidi ya Etou du Sahel, nimeanza kuwapongeza Yanga kwa sababu ya uwezo ulioneshwa na Etou du Sahel, kiufupi naamini kila mmoja atakuwa na mtazamo wake kuhusu mechi hiyo, kuna watu wanasema kukosekana kwa Salum Telela lilikuwa pengo kubwa na wengine wanasema yao pia.
Lakini kikubwa ni kuifanyia tathmini mechi yenyewe, wakati kabla haijaanza tulikuwa tumekaa pamoja na Emmanuel Arnold Okwi, ikaletwa listi ya vikosi vitakavyoanza na wachezaji wa akiba, mmoja kati ya wachezaji ambao aliwaonesha kuwa ni hatari ni anayevaa jezi namba 12 ambaye ni Franck Kom, akasema kuwa alimuacha wakati anaondoka Etou du Sahel, na tulilithibitisha hilo baada ya mpira kuanza, jamaa alitawala ile mbaya sehemu ya kiungo, alikuwa anafanya anachotaka, ana nguvu, ana kasi, na mpira anaujua.
Najiuliza hata angekuwepo Salum Telela je angeweza kupambana na huyu mtu ambaye anacheza easy game huku akitumia nguvu panapostahili.
Tukiangalia pia timu nzima ya Etou du Sahel kiujumla walikuwa vizuri sana kuliko Yanga, walitawala mchezo, walijiamini, walitumia ukubwa wa miili yao kufanya blocking,  walitumia vizuri vimo vyao katika mipira ya vichwa, hili liliwafanya Yanga wapoteze mipira Mingi na kutoka mchezoni kipindi cha kwanza,   lakini hata kipindi cha pili baada ya waarabu kurudisha goli Yanga walijaribu ku
tulia ili wapate bao la ushindi lakini bado mambo yalikuwa magumu mno.
Nachokusudia hapa ni kwamba kumekuwa na kasumba ya watanzania kulalamika siku zote kuwa tukienda kucheza na waarabu tunaonewa, mimi pia nakubaliana na fact hiyo, lakini bado nina wasiwasi na uwezo wa timu zetu, tumeshashuhudia mechi nyingi ambazo waarabu wamekuja kucheza hapa, tunajiona kabisa kuwa uwezo wetu kwa hawa jamaa tupo chini, mfano mzuri ni mechi ya jana tu, kila mtu ameona jinsi waarabu wameonesha wamelelewa kisoka, wamafanya wanachokitaka, na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja walikuwa wako juu.
Tuangalie pia hata timu yao ya taifa ya Tunisia imeshiriki kombe la mataifa ya Afrika mara ngapi na sisi tumeshiriki mara ngapi?, ubora wa ligi yao ndio umewafanya washiriki mara nyingi kombe la mataifa ya Afrika, lakini bado tunataka kuamini vilabu vyetu ni bora kuliko wao, hivi ni kweli?
Ukitazama hata mazingira ya timu, mishahara ya wachezaji  wao ipo juu. Mpira unahitaji uwekezaji na sio blaa blaa tu. Mpira ni mchezo wa wazi hauchezwi chumbani, unachezwa uwanjani kila mtu anaona, tuache utamaduni wa kusifiana ujinga, tuhamasishane kuwekeza katika soka na kuwa na malengo ya mbali .
Etou du Sahel wametuumbua kwa kuonesha kuwa soka lao lipo juu, na walilazimisha matokeo ya mechi. Tusubiri mechi ya Marudiano pengine Yanga watanifanya nionekane muongo katika uchambuzi wangu kwa kuwatoa waarabu.

Advertisement

 
Top