Ingawa walitangulia na kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya FC Platnum, Yanga wameonywa kuwa makini sana.
Yanga ilishinda kwa mabao 5-1 katika mechi ya kwanza ya Shirikisho dhidi ya FC Platnum jijini Dar. Yanga inaondoka kesho kuwafuata Wazimbabwe hao.
Lakini baadhi ya Watanzania wanaoishi jijini Harare Zimbabwe wameonyesha kuwa na hofu na Wazimbabwe hao kwamba watatumia nguvu nyingi katika fitina.
Shabani Msonga na baadhi ya Watanzania wanaoishi jijini Harare wamesema Wazimbabwe hao watafanya kila njia nje na ndani ya uwanja kuivuruga Yanga.
"Baadhi ya mashabiki wa Yanga wameondoka usiku huu kutoka hapa Harare kwenda Bulawayo. Tumezungumza nao na kuwaeleza hali halisi.
"Kwamba wauambie uongozi wa Yanga kuwa makini sana kwa kuwa fitina ndiyo zitawaongoza Wazimbabwe kule Bulawayo.
"Tena utaona uwanja wa kule kijijini na wameamua kwenda mgodini kabisa ili waweze kufanya wanachotaka," alisema Msonga.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga ulishatoa kauli na kusema utapambana na kila fitina na uko tayari.