MVUA zimeendelea kunyesha mjini Shinyanga na kuvuruga mechi mbili za ligi kuu Tanzania bara.
Jumamosi ya wiki iliyopita, Kagera Sugar walitakiwa kuchuana na Simba kwenye uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga, lakini mechi hiyo iliahirishwa kutokana na uwanja wa kujaa maji kutokana na mvua iliyonyesha kwa muda mrefu mpaka saa chache kabla ye mechi kuanza.
Mechi hiyo inachezwa leo jioni katika uwanja huu mjini hapa.
Jana jioni pambano la Stand United na Mtibwa Sugar liliaahirishwa baada ya mvua kubwa kunyeshwa dakika 5 tu baada ya mechi kuanza.
Mambo yalikuwa hivi Shinyanga
Muamuzi Ahamad Simba alilazimika kuahirisha mechi hiyo dakika ya 33′ wakati ambao Stand walikuwa mbele kwa goli moja lililofungwa na Haruna Chanongo dakika ya 12 ya mchezo.
Hali ya uwanja wa CCM Kambarage jana jioni
Wakati Simba ikijiandaa kucheza na Kagera Sugar Kocha mkuu wa Wekundu hao wa Msimbazi, Mserbia, Goran Kopunovic amesema ana imani kubwa kikosi chake kitafanya vizuri leo, licha ya kumkosa kiungo wake wa ukabaji, Jonas Mkude.
Mkude alirejea jana Dar es salaam kwa ndege kutokea Mwanza alikoenda jana mchana kwa gari binafsi aina ya Noah na kupanda Ndege saa 11:00 jioni amerudi kwenza kumzika baba yake mzazi aliyefariki dunia juzi.
Kopunovic amesema mvua ndiyo hofu yake kubwa kama zitaharibu uwanja.
“Kucheza katika mazingira ya mvua, kuna ugumu wake. Kama haitakuwa hivyo nina imani tutacheza vizuri tu.
“Kidogo nimekuwa nikiomba, mvua isinyeshe tena . Uwanja ukiwa umetulia ni rahisi kiuchezaji,” alisema Kopunovic raia wa Serbia.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu huku Simba wakitaka kulipa kisasi baada ya Simba kufungwa bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza.
