‘Simba haijawahi kuifunga City tangu timu hiyo ya Jiji la Mbeya ilipokwea ligi kuu ya Bara msimu uliopita.’
MFUPA uliomshinda fisi, mbwa atauweza? Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mbeya City FC kutamba kufanya vyema dhidi ya Simba SC timu ambayo vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa, Yanga SC wamepoteza pointi msimu huu.
Ni Stand United FC pekee iliyovuna pointi nyingi dhidi ya Simba SC msimu huu. Timu hiyo 
pekee ligi kuu ya Bara msimu huu kutoka mkoani Shinyanga inayonolewa na Mganda Mathia Lule, imekusanya pointi 4 kati ya 6 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Stand iliishika Simba SC kwa sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa jijini hapa mzunguko wa kwanza kabla ya kuichapa 1-0 katika mechi ya mzunguko wa pili Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Kocha mkuu wa City, Juma Mwambusi, ametamba kuwa kikosi chake kitaendelea ubabe wa kutopoteza mechi dhidi ya Simba SC tangu kikwee ligi kuu msimu uliopita.
Simba SC na City zilitoka sare ya 2-2 mzunguko wa kwanza kabla ya kutoka suluhu mzunguko wa pili msimu uliopita kisha Mnyama kulala kwa mabao 2-1 nyumbani Uwanjja wa Taifa katika mechi ya mzunguko wa kwanza msimu huu Januari 28.
Je, City itatumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Sokoine jijini Mbeya Jumamosi na kuwa timu ya kwanza kupata pointi zote sita (6) dhidi ya Simba SC msimu huu?
Je, City itailazisha sare timu hiyo ya kocha Mserbia Goran Kopunovic na kuifikia rekodi ya Stand msimu huu na kulinda heshima yake ya kutopoteza mechi dhidi ya mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara?
Tusubiri kesho tuone, lakini tayari benchi la ufundi la Simba SC limeshaweka wazi kwamba limepania kushinda mechi zote zilizobaki ili timu imalize katika nafasi mbili za juu na kupata fursa ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani baada ya kukosekana kwa misimu mitatu mfululizo.

Advertisement

 
Top