BAADA ya kuibuka na ushindi mkubwa dhidi ya Coastal Union FC juzi, Yanga SC wameitaka Mbeya City FC iangalie tarehe kwa kuwa idadi ya mabao wanayofunga kwa sasa hulingana na terehe ya siku husika.
Yanga SC, mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara na wawakilishi pekee wa nchi waliosalia katika michuano ya kimataifa ya klabu mwaka huu, walitoa kipigo kikubwa cha mabao 8-0 dhidi ya Coastal katika mechi ya Ligi Kuu ya Bara Uwanja wa Taifa jijini hapa, ikiwa ni siku ya Jumatano Aprili 8.
Kikosi cha Mdachi Hans van der Pluijm cha Yanga SC, kitashuka Uwanja wa Taifa Jumapili Aprili 12, kuikabili timu iliyopunguza makali yake ya msimu uliopita, Mbeya City FC katika mwendelezo wa ligi hiyo huku uongozi ukitamba kuwa City itafuata nyayo za ‘Wagosi wa Kaya’ kwa kubamizwa mabao mengi.
Pluijm aliumbia mtandao huu jana jioni mara tu baada ya mazoezi ya kikosi chake Uwanja wa Karume jijini hapa kuwa mechi za Ligi Kuu dhidi ya Coastal na City ni sehemu ya maandalizi yao kabla ya kuikabili Etoile Sportive du Sahel (ESS) katika michuano ya kimataifa.
Kutokana na kipigo cha mabao 8-0 kuangukia Aprili 8 (juzi), Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro, amesema jijini hapa kuwa City inapaswa kuangalia tarehe ya mechi yao inayofuata kisha ijiandae kupokea idadi ya mabao ambayo ametamba itakuwa sawa na tarehe husika.
“Coastal tumewafunga mabao 8-0 tarehe nane, Mbeya City kabla ya kututangazia vita sisi (Yanga SC), wanapaswa kuangalia tarehe ya mechi yetu dhidi yao. Tutawapiga mabao 12 Jumapili maana tuna wachezaji wenye uwezo huo. Yanga hii ni ya kimataifa.
Wazitangazie vita timu za mchangani na siyo Yanga ya uongozi wetu huu ya kimataifa,” ametamba Muro.
Wazitangazie vita timu za mchangani na siyo Yanga ya uongozi wetu huu ya kimataifa,” ametamba Muro.
Baada ya kuishika Azam FC kwa sare ya 1-1 Uwanja wa Azam jijini juzi na kuwagombanisha Meneja wa Azam FC, Jemedari Said na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Saad Kawemba, kocha mkuu wa City, Juma Mwambusi, aliwataka wachezaji wake wajiandae kwa vita dhidi ya Yanga SC Jumapili.
Mwambusi, kocha bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopita, alisema: “Nashukuru wachezaji wangu wamepambana, tumepata pointi moja ni jambo zuri kwetu kwa sababu tutakuwa tumesogea katika nafasi nyingine, tuna mchezo Jumapili, hivyo tujiandae na tujue kuwa tunatakiwa kuipigania timu yetu mpaka dakika ya mwisho.”
Yanga SC iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 43 baada ya mechi 20 wakati City iko nafasi ya saba ikiwa na pointi 25 baada nayo kushuka dimbani mara 21.