Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amewatoa hofu mashabiki na wanachama wa timu yake kwamba atasajili winga hatari kuziba pengo la Mrisho Ngassa anayetimkia Free State Stars ya Afrika Kusini.
Ngassa ambaye mkataba wake umeisha siku chache zilizopita, muda mrefu alikuwa ameshasaini kuichezea timu hiyo ya Afrika Kusini na alibaki nchini kumalizia muda wa kuitumikia Yanga.
Pluijm, raia wa Uholanzi amesema, mashabiki wasiwe na hofu kuhusu kuondoka kwa Ngassa kwani hakuna ubaya wowote kwa mchezaji kuondoka, isipokuwa wanatakiwa kumuombea maisha mema aendako.
“Sina hofu yoyote kuhusu kuondoka kwa Ngassa, japokuwa ni mchezaji mwenye uwezo mzuri na unayeweza kumtegemea kikosini, lakini hakuna jinsi, ni lazima aondoke, ingekuwa ngumu kumzuia.
“Mashabiki waondoe hofu kwani timu ndiyo inaingia katika kipindi cha usajili ambacho tutasajili mchezaji kama Ngassa uwanjani lakini huyo mpya atakuwa hatari zaidi,” alisema Pluijm.
Katika mchezo dhidi ya Azam FC katikati ya wiki hii, Ngassa alitumia muda mwingi kuwaaga mashabiki wa Yanga baada ya mchezo huo ambao Azam ilishinda mabao 2-1.