‘Kiongera alalazimika kusimamisha mkataba wake na Simba ili aende India kufanyiwa upasuaji wa goti mwishoni mwa mwaka jana.’
UONGOZI wa Simba umesema umeamua kumrejesha kundini mshambuliaji wake Mkenya Raphael Kiongera baada ya kuridhika na vitu anavyovifanya katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kwa sasa.
Kiongera kwa sasa anaitumkia KCB kwa mkopo akitokea Simba baada ya kupona majeraha yake ya goti.
Zacharia Hanspope, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, amesema jijini hapa muda mfupi uliopita kuwa wamekuwa wakifuatilia kwa kina maendeleo ya Kiongera na sasa wameamua kumrejesha katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu ujao.
“Kiongera ni mchezaji wetu, tumejiridhisha kwamba amepona vizuri maana sasa anacheza zaidi ya dakika 70. Tunamrudisha hapa Tanzania kwa ajili ya kikosi chetu cha msimu ujao,” amesema Hanspope.
Kiongera aliumia goti la mguu wa kulia katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa Septemba 21, 2014 na kumlazimu kukaa nje ya uwanja kwa miezi mingi.