Kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars' wakati kikijifua Addis Ababa, Ethiopia
Kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ wakati kikijifua Addis Ababa, Ethiopia
Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kucheza mechi yake ya ugenini dhidi ya Misri siku ya Jumapili Juni 14 mwaka huu kwenye uwanja wa Borg El Arab uliopo jijini Alexandria kwa ajili ya kuwania kufuzu kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).
Kwenye mechi hiyo wakati Stars ikikabiliana na Mafarao mashabiki hawataruhusiwa kuingia uwanjani kutokana na baadhi ya vitendo vya vurugu ambavyo vimekuwa vikitokea kwenye baadhi ya viwanja pindi michezo ya kandanda inapokuwa inapigwa. Shirikisho la soka la Afrika (CAF) na chama cha soka nchini Misri vimekuwa vikikataza mashabiki kuingia uwanjani wakati timu zinapokuwa zikicheza ili kuzuia vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikihatarisha maisha ya watu wanaojitokeza kushuhudia michezo hiyo.
Kwa maana hiyo mechi kati ya Taifa Stars dhidi ya Misri itakayopigwa kwenye dimba la Borg El Arab itapigwa bila ya kuwepo kwa mashabiki. Stars inatarajia kuondoka kwa ndege kutoka Ethiopia majira ya saa 4:00 sawa na saa 5:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na inategemea kuwasili Cairo Misri saa 7:00 usiku sawa na saa 8:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki. Baadaye wataunganisha hadi jijini Alexandria ambapo ndipo mechi itakapofanyika.
Ikumbukwe kikosi cha Stars kiliweka kambi ya takribani juma moja jijini Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kujiandaa na mechi yake ya Jumapili ambapo itakuwa na kibarua cha kuwakabili ‘Mafarao’ timu ya taifa ya Misri.
Kwa taarifa tulizonazo ni kwamba, kiungo Amri Kiemba atasafiri moja kwa moja kuelekea Misri kuungana na kikosi cha Taifa kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa ambaye anakabiliwa na majukumu binafsi.

Advertisement

 
Top