
Nahodha wa Azam FC John Bocco (kulia) akikabidhiwa kombe la Kagame na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Meck Sadick na Raila Odinga baada ya mchezo wa fainali walioshinda kwa goli 2-0 dhidi ya Gor Mahia
Azam wametangazwa kuwa mabingwa wapya wa kombe la Kagame lilinaloshirikisha vilabu bingwa vya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuibwaga timu ya Gor Mahia ya Kenya kwa goli 2-0 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa leo jioni kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Azam yamezamishwa wavuni na John Bocco aliyefunga goli la kwanza na Kipre Tchetche akamaliza matumaini ya Gor Mahia kutwaa taji hilo kwa mara ya tano baada ya kuifungia Azam goli la pili na la ushindi kwenye mchezo wa leo.

Azam FC walipata goli la kwanza dakika ya 16 kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao John Bocco akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Kipre Tchetche aliyewatoka walinzi wa Gor Mahia kisha kuachia krosi iliyomkuta Bocco ndani ya boksi la Gor Mahia na kuupachika mpira wavuni kuiandikia Azam goli la kuongoza

Kipindi cha pili kilipoanza, Azam walifanya mabadiliko kwa kumtoa Shah Farid Mussa na kumuingiza Erasto Nyoni
Daika ya 50 kipindi cha pili Azam FC walifanya shambulizi kali ambapo Kipre Tchetche aliwatoka mabeki wa Gor Mahia na kuachia shuti kali lililogonga mwamba wa pembeni na kutoka njeya uwanja.

Azam walifanya mabadiliko tena ambapo dakika ya 68 walimtoa Ame Ally ‘Zungu’ akaingia Frank Domayo na dakika ya 88 Kipre Tchetche akapumzishwa kumpisha Didier Kavumbagu.
