
Emanuel Memba (kulia) wa Kauzu FC akiwania mpira na beki wa Friends Rangers Mgaya Juma wa Friends Rangers wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Ndondo Cup
Timu ya Kauzu FC ‘Wauza mitumba wa Tandika’ leo imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya Sports Xtra Ndondo Cup baada ya kuchomoza na ushindi wa penati 4-2 dhidi ya timu ya Friends Rangers ya Magomeni-Kagera kwenye mchezo wa robo fainali ya michuano hiyo ulipoigwa kwenye uwanja wa Bandari, Tandika jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo uliomalizika bila kupata mbabe ndani ya dakika 90 ilibidi uamuliwe kwa mikwaju ya penati na hapo ndipo Kauzu wakafanikiwa kukata tiketi ya kucheza fainali ya Ndondo Cup kwa msimu huu wa mwaka 2015.
Siku ya Ijumaa utachezwa mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya Makumba FC iliyopoteza kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza mbele ya Faru Jeuri hivyo itakutana na walipoteza mchezo wa leo ambao ni Friends Rangers.
Jumapili ndio itapigwa mechi ya fainali ambayo imesubiriwa kwa takribani miezi miwili. Faru Jeuri ndio watakuwa wenyeji wa mchezo huo kutokana na kutangulia kufuzu kwenye hatua ya fainali wakiwakaribisha Kauzu FC kwenye uwanja wa Bandari.