Azam
FC imeanza vizuri michuano ya Kombe la Shirikisho ya Caf kwa kuitwanga
Bidvest Wits ya Afrika Kusini mwa mabao 3-0 ikiwa nyumbani kwao Afrika
Kusini.
Azam FC ambayo ilitua nchini humo siku tatu zilizopita, ilikwenda mapumziko na sare ya bila kufungana dhidi ya wenyeji wake.
Azam
FC ambao walianza kipindi cha kwanza kwa tahadhari kubwa walionekana
kubadilika katika kipindi cha pili na kushambulia mfululizo hadi
walipopata bao katika dakika ya 51 kupitia Salum Abubakary ‘Sure Boy’
aliyepiga shuti kali nje ya 18.
Wakati
Wits wanajiuliza, Azam FC haraka ilipata bao la pili kupitia Shomari
Kapombe ambaye alifanya juhudi kulala chini na kuuwahi mpira wa krosi
aliousukumiza wavuni.
Bao
la pili la Azam FC lilionekana kuwachanganya Wits, Azam FC wakaitumia
nafasi hiyo kusukuma mashabulizi mfululizo na dakika ya 59, ikaandika
bao lake la tatu kupitia kwa nahodha John Bocco, ‘Adebayor’.
Dakika
ya 73, kocha Stewart Hall alimtoa Didier Kavumbagu na nafasi yake
ikachukuliwa na Khamis Mcha, dakika ya 79 akamtoa Kapombe na kumuingiza
Waziri Salum na dakika ya 83 akamtoa Kipre Bolou na nafasi yake
akaichukua Frank Domayo.