KLABU
Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo saa 3.00 usiku kwa saa
za Afrika Mashariki itakuwa na shughuli pevu pale itakapokuwa
ikikabiliana na wenyeji wao Esperance de Tunis katika mchezo wa
marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Mchezo
huo wa raundi ya pili ya michuano hiyo utafanyika katika Uwanja wa
Olympique de Rades na Azam FC inahitaji ushindi wowote au sare yoyote
ili kusonga mbele kutokana na ushindi wa mabao 2-1 walioupata jijini Dar
es Salaam wiki moja iliyopita.
Mabao ya Azam FC katika mchezo
huo yaliwekwa kimiani na mawinga machachari Ramadhan Singano ‘Messi’ na
Farid Mussa, waliofanikiwa kuonyesha kiwango kizuri na kuleta madhara
makubwa kwenye safu ya ulinzi ya Esperance.
Wachezaji wa Azam FC
wana morali kubwa kuelekea mchezo huo, hata katika mazoezi ya juzi na
jana wameonekana kufanya kwa ari kubwa na bidii jambo ambalo linaonyesha
kila dalili kwa timu hiyo kupata matokeo mazuri kesho.
KAULI YA BENCHI LA UFUNDI
Akizungumzia
namna walivyojipanga kwa mchezo huo baada ya mazoezi ya jana usiku,
Kocha Mkuu wa Azam FC Stewart Hall, amesema kuwa wachezaji wana hali
nzuri kuelekea mechi hiyo huku akiamini ya kuwa watapata matokeo mazuri.
“Uwanja
ni mzuri sana, wachezaji nao walivyouona kwa mara ya kwanza wameukubali
mno, sehemu ya kuchezea ni nzuri kwa ajili ya mpira kuchezwa, inaruhusu
mpira kuchezeka haraka, mpira utakuwa ni haraka sana kutokana na nyasi
za uwanja kuwa fupi, hivyo kutakuwa na mpira mzuri sana kesho (leo),”
alisema.
Hall alisema kuwa wanatarajia kufanya kazi nzuri licha
ya kuwakosa baadhi ya wachezaji wake wanaosumbuliwa na majeraha akiwemo
beki Shomari Kapombe ambaye ni mgonjwa.
“Tunatakiwa kukabiliana
na hali hiyo kwa kufanya kazi yetu kwa bidii uwanjani, pia lazima
tujipange vizuri ili kupata matokeo tunayoyataka, najua kikosi changu
kitaathirika kwa kuwakosa wachezaji hao, lakini tupo tayari kwa
mapambano,” alisema.
Kocha huyo wa zamani wa Zanzibar Heroes na
Sofapaka ya Kenya, aliongeza kuwa: “Jambo kubwa tunalotakiwa kuhakikisha
kesho (leo) ni kuwa vizuri katika eneo la ulinzi na iliyopangika
vizuri, baada ya hiyo hapo ndipo utapata msingi mzuri kuelekea maeneo
mengine uwanjani, unajua unapojenga nyumba huwezi kuanza kuweka paa
kwanza lazima uanze na msingi, ambapo jambo kubwa la kukuwezesha
kushinda kwenye mpira ni kujenga vema eneo la ulinzi.”
WACHEZAJI NAO WALONGA
Nahodha
wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amesema wamemaliza vema maandalizi
ya mchezo huo huku akidai kuwa kila mchezaji ana morali kubwa kuelekea
mchezo huo.
“Mazoezi
ya mwisho leo (jana) yalikuwa mazuri tumemaliza salama, yalikuwa na
morali kubwa kilichobaki ni wachezaji kwenda kujituma tu uwanjani kesho
(leo) na Mungu atatusaidia sisi kupambana na kuweza kupata matokeo
mazuri, lakini tunaiheshimu Esperance kuwa ni timu kubwa,” alisema.
Naye
mshambuliaji nyota kutoka Burundi Didier Kavumbagu, amesema kuwa
wamejipanga kuweza kukabiliana na yote watakayokutana nayo uwanjani leo
na kuweza kupata matokeo wanayoyahitaji.
“Azam FC mpaka sasa
ninapozungumza tunanafasi kubwa ya kusonga mbele, lakini yote itatokana
na namna tutakavyocheza mchezo wa kesho (leo), lakini ni lazima
wachezaji tujitume kwa moyo wetu wote na kuwa kitu kimoja uwanjani na
kupigana kwa namna tulivyopigana katika mchezo wa kwanza pamoja na
kuzidisha bidii zaidi ili tuweze kufuzu,” alisema.
Kwa upande
wake mfungaji wa bao la ushindi kwenye mchezo wa Dar es Salaam, Ramadhan
Singano ‘Messi’, alisema kuwa wanaamini ya kuwa kwa uwezo wa Mwenyezi
Mungu kesho (leo) watapata matokeo yale ambayo timu inayategemea pamoja
na Watanzania kwa ujumla.
“Mimi kwa timu yoyote ambayo tunakutana
nayo huwa najiandaa vizuri, na hata huo wa kesho (leo) nao nitajiandaa
vizuri ili kuwapa faida timu yangu ya Azam, Mwenyezi Mungu anajua sisi
tunanafasi gani katika mchezo huo, ila naamini tutafanya vizuri,”
alisema Singano.
REKODI MPAKA SASA
Azam FC imefanikiwa kufunga
mabao tisa na kufungwa manne mpaka sasa katika mechi tatu za michuano
hiyo walizocheza mpaka sasa, saba wakifunga ilipocheza na Bidvest Wits
ya Afrika Kusini na kuitoa kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-3 na mawili
walipoichapa Esperance 2-1 jijini Dar.
Katika mechi zote hizo
tatu, Azam FC haijafungwa mchezo wowote ikiwa na ushindi wa asilimia 100
na anayeongoza kuifungia mabao ni Kipre Tchetche, aliyefunga matatu
mpaka sasa na nahodha Bocco akifunga mawili ndani ya michuano hiyo.
NIDHAMU JUU AZAM FC
Hadi
Azam FC inacheza mchezo wa nne leo wa michuano hiyo, hadi sasa ni
miongoni mwa timu zenye nidhamu kubwa ya mchezo kutokana na kukusanya
kadi mbili tu za njano huku ikiwa haina kadi yoyote nyekundu.
Kadi
hizo zote za njano amezipata kiungo mkabaji raia wa Rwanda, Jean
Baptiste Mugiraneza, ambaye ataukosa mchezo huo kwa kukusanya idadi hizo
za kadi, lakini wapinzani wao Esperance mpaka sasa wamekusanya kadi
nane za njano.
HATUA IJAYO ITAKAVYOKUWA
Azam FC ikifanikiwa
kusonga mbele itafuzu kwa hatua ya mwisho ya mtoano (play off), huko
itapangiwa moja ya timu nane zilizotolewa kwenye raundi ya mwisho ya
mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikipenya hapo tena itaenda moja kwa
moja katika hatua ya makundi (robo fainali).