BAADA ya kuifumua 3-1 Mtibwa Sugar, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC wanatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kesho kwenda Kampala, Uganda kuweka kambi ya siku 10 kujiandaa kwa mechi zinazofuata za ligi hiyo.
Azam FC waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Kikosi cha Mecky Mexime cha Mtibwa Sugar katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam jijini jana usiku kupima uwezo wa taa za kisasa zilizowekwa kwenye uwanja huo.
                  
Mabao ya Azam FC yalifungwa na mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu (mwenye mabao manne VPL), beki wa kati Aggrey Morris (mwenye mabao mawili VPL) na mshambuliaji Khamis Mcha ‘Vialli’ huku mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ (mwenye mabao mawili VPL) akiwafuta machozi wageni Mtibwa Sugar, mabao yote yalifungwa kipindi cha kwanza.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba amesema kuwa ziara hiyo ni maalum kwa timu kujiandaa kwa mechi zinazofauta za VPL na kikosi kitarejea Desemba 22, yaani siku tano kabla ya kuivaa Yanga katika mechi yao ya raundi ya nane ya VPL msimu huu.
Ligi hiyo iliyosimama kwa muda Novemba 9, baada ya mechi za raundi ya saba kucheza, inatarajiwa kuanza tena Desemba 26.
Azam FC imefanya usajili wa wachezaji wawili tu katika dirisha dogo, ambao beki wa kati Serge Wawa Pascal, raia wa Ivory Coast aliyekuwa anacheza El Merreikh ya Sudan na kiungo Amri Kiemba aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka Simba.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara ambao pia wamealikwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanziba mwakani, wamemchukua kocha Mganda George ‘Best’ Nsimbe kuziba pengo la Muingereza Kali Ongala aliyejiuzulu baada ya mechi sita.
Azam FC wako nafasi ya pili katika msimamo wa VPL kwa sasa wakiwa na pointi 13 sawa na Yanga SC walioko nafasi ya tatu, pointi mbili nyuma ya vinara Mtibwa Sugar ambao hawajafungwa mechi hata moja VPL msimu huu.





Advertisement

 
Top