Ukiachana na michezo ya ligi kuu Tanzania Bara, klabu za Simba SC na Yanga michezo baina ya timu hizo hasimu na zenye upinzani wa Jadi nchini Tanzania huwa na msisimko mkubwa. Tunazungumzia ‘ Dar es Salaam-Pacha’, mchezo unaohusisha timu mbili za Ilala, samba wakitokea katikati kabisa ya mji, ‘ Mtaa wa Msimbazi-Kariakoo ‘ na Yanga wakitokea ‘ Mitaa ya Twiga na Jangwani-Kariakoo’ pembeni kidogo ya mji.
                       
Timu hizo hasimu zitapambana siku ya Jumamosi katika uwanja wa Taifa, Dar, katika mchezo wa hisani, Nani Mtani Jembe-2. Achana na mambo ya zawadi pambano hilo ni moja kati ya michezo ambayo inatarajiwa kuwa mkali sana hasa baada ya timu hizo kutofungana katika michezo miwili iliyopita-Yote ya ligi kuu. Mwaka uliopita Simba ilishinda kwa mabao 3-1, mabao mawili ya Amis Tambwe na moja lilifungwana Awadh Juma, wakati bao la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Emmanuel Okwi.
ZIMEKUTANA MARA NNE KATIKA KAGAME CUP-KLABU BINGWA AFRIKA MASHARIKI NA KATI
Nje ya ligi kuu, timu hizo zimekutana mara nne katika michuano ya Kagame Cup-Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati. Januari, 1975 katika uwanja wa Nyamagana, Mwanza mabao ya Geilson Sembuli na Sunday Manara yaliwapa ushindi wa maba 2-0 Yanga , na baada ya miaka 18 timu hizo zilikutana tena katika mchezo wa fainali na safari hii Simba ilishinda ubingwa huo baada ya kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare ya kufungana bao 1-1 katika uwanja wa Aman, Zanzibar, Januari, 1992.
Kwa mara ya tatu ratiba ya michuano hiyo iliwagonganisha mahasimu hao katika mchezo wa kusaka mshindi wa Tatu, 2008 lakini Yanga haikutokea katika uwanja wa Taifa na Simba wakapewa ushindi wa mezani. Mara mwisho timu hizo zilipokutana katika michuano hiyo ilikuwa ni katikati ya mwaka, 2011 na Yanga walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Mghana, Keneth Asamoah katika uwanja wa Taifa.
KOMBE LA HEDEX………….
June 30, 1996, Bakari Malima ‘ Jembe Ulaya’ alifunga bao la kwanza, kisha winga Edibilly Lunyamila akapiga bao lingine na kutengeneza ushindi wa mabao 2-0 na Yanga wakatwaa ubingwa wa Michuano ya Hedex katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kwani timu hizo ziliporudiana wiki mbili baadaye katika uwanja wa Uhuru, zilifungana bao 1-1. Hussein Marsh alifunga kwa upande wa Simba kwa mkwaju wa penalti. Bakari Malima alifungakwa mara nyingine ndani ya wiki mbili dhidi ya Simba. Mchezo wa marudiano ulipigwa Julai 13 katika uwanja wa Uhuru.
TUSKER CUP……….
Mbele ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Ally Hassani Mwinyi mashabiki wenye hasira wa Yanga walianzisha vurugu kubwa hasa wakipinga maamuzi ya mwamuzi Omar Abdulkadir ambaye alikubali bao la Madaraka Suleimani ‘ Mzee wa Kiminyio’ katika dakika ya 32.
Akicheza kwa mara ya kwanza, Mkenya Mark Sirengo aliifungia Simba bao la kuongoza katika dakika ya Tatu tu ya mchezo, lakini kiungo-mshambulizi, Sekilojo Chambua aliisawazishia timu yake ya Yanga katika dakika ya 16. Madaraka alifunga bao hilo baada ya kutumia mkono kutengeneza mpira kisha kufumua shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari. Abbas Tariba ambaye alikuwa kiungozi wa juu wa Yanga alitoa hishara kwa wachezaji wa timu yake kutoka uwanjani kwa madai ya kuonewa na mwamuzi.
Baada ya purukushani hizo mchezo uliendelea na Yanga walikubali bao hilo. Sirengo alifunga kwa mara ya pili huku likiwa bao la Tatu kwa Simba katika dakika ya 76 kisha Emmanuel Gabriel akafunga bao la mwisho zikiwa zimesalia dakika saba mchezo kumalizika na kuipatia Simba ushindi wa kwanza mkubwa katika ‘ karne ya 21’ dhidi ya mahasimu wao. Simba ilishinda kwa mabao 4-1 na kutwaa ubingwa wa kwanza wa michuano hiy, Februari 10, 2001.
Kwa mara ya pili timu hizo zilikutana katika fainali, Julai 2, 2005 katika uwanja wa CCM Kirumba na Simba ilifanikiwa kushinda kwa mabao 2-0 na kutwaa ubingwa huo. Emmanuel Gabriel alifunga bao la kwanza katika dakika ya 60 kisha Mussa Hassan Mgosi akafunga bao la pili dakika 12 baadae.
Yanga ikiwa haijaishinda katika michuano ya Tusker ilikutana tena na wapinzani wao hao katika mchezo wa nusu fainali wa michuano hiyo, Agosti, 15 katika uwanja wa Taifa. Gabriel alifunga bao la kuongoza kwa Simba katika dakika ya 69, kabla ya kiungo, Credo Mwaipopo kuisawazisha Yanga katika dakika ya 90 na kufanya mchezo huo kuingia katika muda wa ziada, kisha mikwaju ya penalti baada ya mshindi kushindwa kupatikana katika muda wa dakika 120. Simba ilishinda kwa mikwaju 7-6 .
Mabao ya Jerry Tegete na Shamte Ally yaliwapa Yanga ushindi wa kwanza dhidi ya mahasimu wao katika michuano ya Tusker, 25 Disemba, 2009 katika uwanja wa Taifa. Tegete alifunga bao la kuongoza kwa timu yake katika dakika ya 67, lakini Hillary Echesa aliisawazishia Simba dakika ya 78 na kufanya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya kufungana bao 1-1 na hivyo kulazimika kuongezewa dakika 30 za ziada na katika dakika ya mwisho, Shamte alifunga bao la ushindi na kuipeleka fainali timu yake kisha ikatwaa ubingwa wa kwanza wa michuano hiyo iliyokufa kwa sasa.
MECHI ZA KIRAFIKI…….
Jumanne Tondolo ‘ Shengo’ alifunga bao la kuongoza kwa Simba katika dakika ya kumi, lakini kiungo, Mrundi, Mwinyi Rajabu alisawazisha bao hilo dakika ya 20 na kufanya mahasimu hao kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa kirafiki ambao ulipigwa 19 Januari, 2003 katika uwanja wa Uhuru.
April 20, Yanga iliishinda Simba kwa mabao 3-0 katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, mabao ya lum Kudra Omary dakika ya 30, Herry Morris dakika ya 32 na lile la Salum Athumani katika dakika ya 47 yalitosha kuwapa Yanga ushindi mkubwa zaidi katika kipindi cha miaka 14 sasa dhidi ya mahasimu wao…….


Advertisement

 
Top