Kocha wa Mwandui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ametua Mtaa wa Msimbazi jijini hapa kuzungumza na uongozi wa Simba SC ili aruhusiwe kuwasajili kwa mkopo winga Uhuru Selemani na beki wa pembeni Miraji Adam kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Julio, kocha wa zamani wa Simba SC, amesema jijini Dar es Salaam leo kuwa tayari ameshawasilisha barua kwa uongozi wa Simba SC juu la kusudi lake hilo kisha kuzungumza na Rais wa klabu hiyo Evans Aveva.

“Tupo hapa Leaders Club jijini Dar es Salaam na wachezaji wangu tunajiandaa kwa mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Kama unavyojua msimu uliopita tulifuzu kushiriki Ligi Kuu lakini tukafanyiwa mambo ya ajabu.
“Nimezungumza na Rais wa Simba na kuwasilisha barua yetu ya kuwaomba tuwasajili Uhuru Seleman na Miraj. Kuna wachezaji wanne tunawataka kipindi hiki cha usajili ili kuimarisha timu yetu.
“Wakitupatia sawa, wakitunyima sawa pia maana mimi niko sawa na sala ya (…. anataja maneno ya kidini ambayo si vizuri kuyaandika) katika Dini ya Kiislamu, ukiishiriki sawa, na usipoishiriki hupati dhambi,” amesema Julio.
Timu ya Polisi Morogoro nayo imeingia katika kinyang’anyiro kuchuana na Mwadui FC kumnyakua beki Miraj.

Advertisement

 
Top