
(Dan) Sserunkuma ni moja ya silaha tutakazozitumia Desemba 13 kuinyoa Yanga, hakuna shida sisi (Simba SC) kwa sasa. Tunaimarisha timu.”
Ni kauli ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hanspope aliyoitoa leo baada ya kufanikiwa kumnasa mshambuliaji Sserunkuma wa Gor Mahia.

Sserunkuma anatua Dar es Salaam Jumatano akitokea kwao Uganda, tayari kusaini kandarasi ya miaka miwili kuitumikia Simba SC.
Baada ya kufanikiwa kumnasa mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Hanspope amesema watamtumia katika mechi ijayo ya Nani Mtani Jembe 2 dhidi ya Yanga SC itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Desemba 13.
Aidha, Hanspope ametamba kuwa wako mbioni kunasa wakali wengine wengi watakaowasajili kipindi hiki cha dirisha dogo.
“Sserunkuma ni moja ya silaha zetu, zipo nyingine zinakuja. Subirini muone namna tunavyowafanya Yanga Nani Mtani Jembe,” amesema Hanspope.
Ingawa hakuwa tayari kuwataja wakali wanaowanyatia, mtandao huu unatambua kuwa Simba SC inasaka kwa udi na uvumba saini za kiungo Shaban Nditi, mabeki Salim Mbonde na Abdallah Hassan, watatu hao wote kutoka Mtibwa Sugar.
Simba SC pia inawataka mabeki Nurdin Chona na Salum Kimenya kutoka Prisons na kingo mshambuliaji Deus Kaseke kutoka Mbeya City FC.