MSHAMBULIAJI Emmanuel Okwi anayesifika kwa kuzisumbua timu zinazomsajili kwa kutorejea kambini mapema pindi anapopewa likizo, ameanza kuuchanganya uongozi wa Simba kutokana na kutorejea kwake nchini kujiandaa kwa mechi ya ‘Nani Mtani Jembe 2 dhidi ya Yanga.
Baada ya kusimama kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu Novemba 9, Okwi na wachezaji wengine wa Simba walipewa mapumziko ya wiki mbili lakini Mganda huyo hajarejea nchini kuungana na wachezaji wenzake katika mazoezi yaliyoanza Jumatatu ya wiki iliyopita kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Desemba 13.
“Okwi amechelewa kurejea nchini kwa sababu aliomba ruhusa baada ya kukumbwa na matatizo ya kifamilia akiwea kwao (Uganda) wiki iliyopita,” amesema msemaji wa Simba, Hamphrey Nyasio katika mkutano na waandishi wa habari jijini jana.
Lakini, mwanzoni mwa wiki Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema mchezaji huyo wa zamani wa Etoile du Sahel ya Ligi Kuu ya Tunisia na Yanga, atachelewa kurejea Tanzania kwa vile anajiandaa kufunga ndoa.
Okwi amekuwa na desturi ya kutorejea klabuni kwake kipindi cha sikukuu za Krismas na mwaka mpya, hasa Sikukuu ya Krismas ambayo huazimisha pia tarehe ya kuzaliwa kwake 1992.
Mganda huyo alijiunga na Simba dakika chache kabla ya dirisha la usajili msimu huu kufungwa Agosti 28 akiwakacha Yanga waliokuwa wamechoshwa na utaratibu wake huo wa kutorejea mapema kikosini apewapo likizo na kuamua kutomalizia fedha za usajili wake na kutomlipa mishahara.
Baada ya kurejea Simba, Okwi aliahidi kucheza soka kwa bidii akiwa na kikosi cha wanamsimbazi na kuachana na tabia zake sizizofaa, lakini inaonekana somo halijamuingia vizuri.
Kikosi cha Simba kiko kambini kwenye moja ya fukwe za Jiji la Dar es Salaam na leo jioni itacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya The Epress ya Ligi Kuu ya Uganda kukijiandaa kwa mechi ya Nani Mtani Jembe 2.

Advertisement

 
Top