Leo kumetolewa taarifa ikionekana kama zinaliendesha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo limebariki matumizi ya tiketi za kawaida badala ya elektroniki katika mechi ijayo ya Nani Mtani Jembe 2 baina ya timu hizo.
Simba SC na Yanga SC zitakutana kwa mechi hiyo iliyoandaliwa na wadhaminiwa wa timu hizo, Kampuni ya Bia nchini (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi Desemba 13 kuanzia saa 10:00 jioni.
Katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za Makao Makuu ya TFF zilizopo Posta, Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, amesema wamekubaliana na klabu kutotumia tiketi za kisasa za kielektroniki katika mechi hiyo.
Wambura amesema pambano hilo litasimamiwa na TFF litachezwa kwa dakika 90 tu na kama muda ho hatapatikana msihndi, mikwaju ya penalti itatumika mshindi na marefa watakaolisimamia wanatarajiwa kutajwa leo na Kamati ya Waamuzi ya shirikisho.
“Viingilio vya mechi hiyo ni Sh. 30,000 kwa VIP B, Sh. 20,000 kwa VIP C, 15,000/- kwa viti vya rangi ya chungwa na Sh. 7,000 kwa viti vya bluu na kijani. Tiketi zitakazotumika ni za kawaida na zitauzwa kwenye vituo ambavyo vitatangazwa baadaye,” amesema Wambura.
Alipoulizwa kwa nini wameamua kupuuza agizo la serikali kwa kuzikacha tiketi za elektroniki, Wambura amedai maamuzi hayo yamepata baraka za serikali.
“Tumezungumza na serikali kabla ya kuruhusu matumizi ya tiketi za kawaida katika mechi hiyo moja, tunaamini pia Bunge (lililoagiza matumizi ya lazima ya tiketi za eletroniki) limetaarifiwa juu ya maamuzi hayo. Tutaendelea kutumia tiketi za eltroniki ligi kuu licha huku tukishughulikia changamoto zilizopo,” amesema Wambura.
Juni mwaka huu, serikali iliigiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuiamuru TFF kutumia mfumo wa tiketi za kielektroniki (ETS) kwenye viwanja mbalimbali vya soka nchini ili kudhibiti uhujumu wa mapato ya milangoni.
Aidha, Ripoti ya Kamati Maalum ya Kudhibiti na Kuboresha Mapato ya TFF iliyotolewa Mei 2011 inaeleleza namna mapato ya milangoni yanavyohujumiwa na baadhi ya watendaji wa TFF kwa kushirikiana wadau wa soka nchini kupitia matumizi ya tiketi za kawaida badala ya tiketi za kielektroniki.
Kabla ya kuchezwa kwa mechi ya kwanza ya watani wa jadi msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwenye Uwanja wa Taifa Oktoba 18, Simba na Yanga walikubaliana kwa pamoja kupinga matumizi ya tiketi za elektroniki katika mechi kati yao, lakini jambo hilo lilipingwa vikali na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia.
SIMBA SC, YANGA SC ZAMWAGA WINO
Meneja Udhamini wa TBL, George Kavishe amesema kuwa tayari Simba na Yanga zimesaini makubaliano ya kucheza mechi ya Nani Mtani Jembe 2 ikiwa ni zawadi ya kufungia mwaka kwa mashabiki na kila timu.
Kavishe amesema mechi hiyo ni maalum kuhitimisha kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 iliyoendeshwa kwa kwa zaidi ya miezi miwili kuwapa fursa mashabiki wa timu hizo kuchangia timu zao.
“Kama tulivyoeleza wakati wa uzinduzi, tumetenga Sh. milioni 100, Sh. milioni 40 zikiwekwa kwenye akaunti maalum ya kila klabu. Sh. milioni 20 ni zawadi ya mechi ya Nani Mtani Jembe 2, timu itakayoshinda itapata Sh. milioni 15 na timu itakayofungwa itapata Sh. milioni 5,” amesema Kavishe.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema kuwa hadi jana asubuhi Yanga walikuwa na Sh. milioni 70 huku watani wao wakibakiwa na Sh. milioni 10 kwenye akaunti.
Taji la Nani Mtani Jembe linashikiliwa na Simba ambao waliwafunga mahasimu wao 3-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Desemba 21, mwaka jana, kipigo ambacho kilifukuzisha benchi zima la ufundi la Yanga lililokuwa chini ya kocha mkuu Mholanzi Ernie Brandts, kocha msaidizi mzawa Felix Minziro na kocha wa makipa Mkenya Razak Ssiwa.