SIMBA imedhihirisha kwamba ni mdebwedo kwa wakatamiwa wa Manungu, Turiani, Timu ya Mtibwa Sugar baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-2 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam leo jioni.
                                 
Simba walikuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika ya 23 kupitia kwa kiungo Said Ndemla alipokifungia Kikosi cha Kocha Mzambia Patrick Phiri bao kabla ya wageni Mtibwa Sugar kusawazisha dakika sita baadaye kupitia kwa mchezaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi aliyeunganisha vyema mpira wa krosi murua ya beki wa zamani wa Yanga, David Luhende.
Dakika ya sita ya kipindi cha pili Mtibwa Sugar wanaonolewa na nahodha wao wa zamani na Taifa Stars, mzawa Mecky Mexime, walipata bao la pili kupitia kwa Mgosi.
                                                       chibwa
Bao la tatu la Mtibwa lilifungwa na Mohamed Ibrahim dakika 13 baada ya saa ya mchezo huo akiendeleza makali ya Mgosi aliyefunga mabao mawili kabla ya kumpisha na kwenda benchi.
Mshambuliaji hatari wa Mtibwa Sugar msimu huu, Ame Ally Amour mwenye mabao manne VPL kwa sasa, aliipatia timu yake bao la nne katika dakika ya 80.
Mabao yote manne ya Mtibwa yalitokana na mashambulizi yaliyoanzia nyuma huku wakatamiwa hao wa Manungu, Turiani, km 100 kutoka mjini Morogoro wakicheza soka la kuvutia la pasi fupi fupi.
Baada ya bao hilo, Simba walianza kulazimisha kuingia kwa nguvu ndani ya boksi la Mtibwa Sugar na kupata penalti ambayo Mfungaji Bora wa VPL msimu uliopita, Mrundi Amissi Tambwe aliitia nyavuni akimchambua kipa aliyefungwa mabao matatu katika mechi saba zilizopita za VPL msimu huu, Said Mohamed.

Penalti hiyo ilitolewa baada ya kiungo mtokeabenchini Shaban Kisiga kuangushwa na mabeki wa Mtibwa Sugar ndani ya boksi.
                           
Kabla ya mapumziko, kiungo tishio kwa Yanga, Ndemla aliumia na kuchukuliwa na kiungo Mrundi Pierre Kwizera.
Ijumaa Simba ilitoka suluhu dhidi ya Timu ya The Express ya Ligi Kuu ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa jijini.
                               
Vikosi vilikuwa;
Simba: Ivo Mapunda, William Lucian/ Nassoro Masoud, Issa Rashid, Abdulazizi Makame, Hassan Issihaka, Said Ndemla/ Pierre Kwizera, Awadh Juma, Abdallah Seseme, Amissi Tambwe, Ibrahim Hajibu/ Shaban Kisiga na Twaha Ibrahim/ Ramadhani Singano.
Mtibwa: Said Mohamed, Hassan Mbande/ Hassan Kessy, David Luhende, Dickson Daudi, Ally Lundenga, Henry Joseph, Vicent Barnabas/ Ally Shomari Sharrif, Musa Nampaka, Abdallah Juma/ Ame Ally Amour, Ibrahim Jeba na Mussa Mgosi/ Mohamed Ibrahim.

Advertisement

 
Top