Klabu ya Simba imethibitisha ujio wa beki David Owino wa Gor Mahia katika klabu hiyo ya Msimbazi.
Katibu Mkuu wa Gor Mahia, Chris Omondi (26) alikaririwa na mtandao rasmi wa klabu hiyo jana akieleza kuwa wamepokea ombi rasmi kutoka Simba wakimtaka beki huyo maarufu ‘Calabar’ akafanye majaribio kabla ya kujiunga nao msimu huu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope amethibitisha ujio wa mshindi huyo mara mbili wa tuzo ya beki bora wa msimu wa Ligi Kuu ya Kenya (KLP) David Owino.
“Ni kweli beki Owino anakuja Simba, tumeshakamilisha mipango yote na atafanya majaribio kabla ya kumsajili,” amesema Hanspope.
Kama akifuzu, Calabar aliyezaliwa Aprili 5, 1988 nchini Kenya ataungana na mshambuliaji hatari Dan Sserenkuma ambaye wiki iliyopita aliachana na Gor na kujiunga Simba kwa mkataba wa miaka miwili.
Hata hivyo, Simba italazimika kuachana na mmoja kati ya nyota wake kigeni ili kukidhi matakwa ya Kanuni za Ligi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinazoyaka klabu za ligi kuu kuwa na wachezaji wasiozidi watano wa kigeni. Simba kwa sasa inao Waganda Emmanuel Okwi, Joseph Owino na Sserunkuma na Warundi Amissi Tambwe na Pierre Kwizera.

Advertisement

 
Top