okwi
Kiungo mwenye kasi wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi huenda asiivae leo Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa ligi kuu utakaopigwa Uwanja wa Taifa kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti aliyoyapata juzi Alhamisi akiwa mazoezini kwenye Viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).


Simba ambayo ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo, inakutana na Mtibwa inayoshikilia nafasi ya tano huku timu hizo zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Jamhuri, Morogoro.

Okwi alikiri kuwa afya yake siyo nzuri kutokana na maumivu ya goti aliyopata mazoezini, ambapo bado hajajua kama atacheza dhidi ya Mtibwa Sugar au la. Hata hivyo imeelezwa atajisikilizia leo kuwa hali yake ikoje.

“Hali yangu siyo nzuri, lakini siwezi kusema moja kwa moja kama mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Mtibwa kwamba sitacheza kwa sababu leo (jana) nitaenda mazoezini nitamsikiliza mwalimu kwanza nione atanipangia programu gani.”


Alipoulizwa Dakatari wa Simba, Yassin Gembe kuhusiana na maendeleo ya nyota huyo aligoma kuzungumza kwa madai ya kufuata taratibu za klabu na kumtaka mwandishi amtafute Ofisa Habari, Humphrey Nyansio ambaye hakupatikana

Advertisement

 
Top