Pamoja na kuwa wageni, mashabiki wa Yanga wameiteka sehemu kubwa ya mji wa Bulawayo.
Mashabiki hao, wamekuwa wakionekana sehemu mbalimbali wakiwa na nguo za njano na kijani, wakisubiri mechi ya Yanga dhidi ya wenyeji wake Platnum.
Yanga ilishinda kwa mabao 5-1 katika mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho jijini Dar.
Mashabiki wa FC Platnum wamekuwa wakijiamini kwamba watashinda zaidi ya mabao manne. Lakini muonekano wa kujiamini wa mashabiki wa Yanga unaonekana kuwakatisha tamaa.
Baadhi ya mashabiki wa Yanga wamekuwa wakikatisha maeneo mbalimbali huku wakisisitiza kwamba wamekuja kuwapa kipigo Platnum kwa mara nyingine.
Tayari kikosi cha Yanga kimewasili mjini hapa kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa katika eneo la migodi.