SIMBA SC imegoma kuziacha pointi tatu kwa mara ya pili msimu huu katika uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.
Februari 22 mwaka huu, Mnyama alichezewa sharubu na Stand United kwa kufungwa bao 1-0 na leo hii anacheza na Kagera Sugar katika uwanja huo.
Wakata miwa hao wa Kaitaba wana kumbukumbu ya kuifunga Simba bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyopigwa desemba 26 mwaka jana uwanja wa Taifa, Dar es salaam, Shukurani kwa bao pekee la Atupele Green.
Msemaji wa Simba, Hajji Manara ameuambia mtandao huu kuwa kocha mkuu wa Simba ameshapanga majeshi yake na ameridhishwa na maandalizi ya mechi hiyo.
“Tunacheza na Kagera Sugar leo. Kwanza walitufunga mechi ya kwanza, pili tulifungwa uwanja huu wa CCM Kambarage na Stand United. Hizi ni timu mbili za kanda ya ziwa, leo tunalipa kisasi kwa kuwafunga Kagera na kuvuna pointi tatu uwanja huu”, Amesema Hajji.
“Sizungumzii kimasihara, kocha ametuhakikishia ushindi licha ya kutambua ugumu wa mechi”.
“Tunacheza mechi tukiwa na majonzi makubwa baada ya washangiliaji wetu (Simba Ukawa) kupata ajali jana na watu saba kupoteza maisha”
“Kwa namna ya kipekee tumeguswa mno na kuumizwa na vifo hivyo, hakika tumepoteza watu muhimu katika wakati muhimu”
“Daima klabu ya Simba itawakumbuka, Mwenyezi Mungu awape wapesi ndugu, jamaa na marafiki na marehemu pamoja na wanasimba wote kwa ujumla”. Ameongeza Hajji.
