11165069_927757313933469_6640690287012942628_n
MOJA ya stori kubwa kwasasa nchini Tanzania ni kitendo cha kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa kusaini mkataba wa miaka minne (4) kuichezea klabu ya Free State Stars inayoshiriki ligi kuu nchini Afrika kusini.
Mkataba huo mnono umesainiwa jana ‘Bondeni’ baada ya pande zote mbili kufikia makubaliano.
Mtandao huu umefanya jitihada za kumtafuta Ngassa na kufanya naye mahojiano maalumu;
Swali: Umekuwa na safari ndefu ya kutafuta timu nje ya nchi na wakati mwingine ulizitosa ofa, pia ulishindwa kufuzu majaribio kama ilivyotokea West Ham na kwingineko, lakini sasa umesaini Free Stars Stars, unasikiaje kufikia mafanikio hayo?
Ngassa: Kwanza kabisa namshukuru mwenyezi Mungu kwasababu malengo ambayo niliyapanga naona yanaanza kutimia, najisikia vizuri.
Swali: Umesaini mkataba mrefu wa miaka minne, ina maana utacheza kwa kipindi chote klabuni hapo au kuna kipengele kinachoruhusu kuuzwa timu nyingine?
Ngassa: Mkataba wangu wa miaka minne sio kwamba nitamaliza yote hapa hapa, hapana!, kama itatokea timu nyingine labda ikafika ofa, wanaweza kuniuza, kuna kipengele kinachoeleza kuwa kama timu nyingine inaweza kutokea naweza kuuzwa.
Swali: Mapokezi yakoje?
Ngassa: Namshukuru Mungu, mapokezi ni mazuri sana!
Swali: Baada ya kusaini mkataba utaendelea kuwepo Afrika kusini au utarudi kwanza nyumbani Tanzania?
Ngassa: Leo nitaungana na timu ya taifa (Taifa Stars), nitaenda Hotelini ambapo watafikia.
Swali: Wewe ni mtu wa familia, je utaiacha familia yako Tanzania?
Ngassa: Kwa mkataba niliosaini natakiwa kuja na familia, kweli nashukuru Mwenyezi Mungu.
Swali: Kwa mafanikio uliyofikia, bila shaka kuna watu wengi wamechangia, lakini ni akina nani ambao huwezi kuwasahau?
 Ngassa: Nashukuru timu zote nilizoweza kupita hadi kufikia hapa. Nimeanza safari ndefu toka nikiwa mdogo, kuna watu wengi wametoa mchango wao mpaka kufikia hapa, kwahiyo nashukuru timu niliyoanzia ya Toto Africans, nikaja Kagera Sugar, nikaja Yanga, nikaenda Azam na baadaye nikaenda Simba na baadaye nikarudi Yanga ambako nimeweza kupata ubingwa, namshukuru mwenyezi mungu kwa yote hayo.
Swali: Kucheza soka la kulipwa katika ligi kubwa ya Afrika kusini maana yake umekuwa nembo ya Tanzania, utatumiaje nafasi hiyo kupeperusha bendera ya nchi yako na kuwa chachu ya wengine waliopo nyuma yako kuja huko?
Ngassa: Kikubwa najua nawakilisha nchi yangu ya Tanzania, najua nawatangaza ambao wako nyuma yangu kama walivyofanya waliopita mfano huku alipita Nteze John, pia kama ilivyo kwa akina Samatta (Mbwana) waliopo nje, ikitokea nafasi nyingine nitasapoti watanzania wengine waje, mtu kama Simon (Msuva), Mkude (Jonas) au Domayo (Frank) na wengine ili tuweze kuungana labda timu moja.
Swali: Free State Stars wameanza kuiwinda saini yako kwa muda gani?
Ngassa: Hawa jamaa toka tunacheza Challenge Uganda walikuwa wananifuatilia, walishaongea sana na Yusuf (Bakhresa) nikiwa Azam, tena kipindi hicho ikaja ofa nyingine ya El Merreikh, walianza kunifuatilia toka zamani sana pamoja na Bocco (John).

Advertisement

 
Top