Mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma, amejutia mno kadi yake nyekundu aliyopewa kwenye mechi dhidi ya Gor Mahia ya Kenya na akakiri kuwa, yeye ndiyo chanzo cha Yanga kufungwa lakini upande wa pili hali imekuwa tete baada ya makocha kumponda kwa alichokifanya.


Ngoma alizawadiwa kadi ya pili ya njano kabla ya kuonyeshwa nyekundu na kwenda nje kwenye dakika ya 23 baada ya kumsukuma Haruna Shakava wa Gor. Kabla ya hapo, Ngoma alikuwa mwiba kwa safu ya mabeki wa Gor kutokana na usumbufu aliokuwa nao na kusababisha bao la kuongoza kwa timu hiyo mapema dakika ya nne.

Hata hivyo, baada ya hapo Yanga ilionyesha wazi kuwa na upungufu uwanjani na mwisho wa siku, Gor wakaibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo huo wa kwanza wa Kombe la Kagame uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Kuhusiana na hilo, mara baada ya mechi hiyo kwisha Ngoma alikiri kuidhoofisha Yanga baada ya yeye kutoka lakini akapiga moyo konde na kusema kuwa ana imani watafanya vizuri kwenye mechi zijazo na watasonga mbele kwa kishindo.

“Wanisamehe sana, sikupenda iwe hivi lakini imetokea, sijisikii vizuri kwa kuwa nimekuwa sababu ya Yanga kufanya vibaya kwenye mechi ya kwanza, upungufu wa wachezaji uwanjani kwa timu kama Gor ilikuwa ni kigezo cha kwanza kuzidiwa.

“Nimeona wachezaji wenzangu walivyopambana lakini imeshindikana, ila naiamini sana timu yangu, ingawa tumepata matokeo mabaya ya kwanza, bado tuna mechi mkononi na najua tutafanya vizuri, tutasonga mbele.”

Kocha wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm naye aliikosoa kadi hiyo kwa kusema wazi kwamba kwa mchezaji profesheno kama Ngoma hakusatahili kufanya makosa kama yale lakini kwa kuwa imeshatokea hana la kufanya.

“Kilichotokea hakikuwa sawa kulingana na maamuzi aliyoyachukua Ngoma, yeye kama mchezaji profesheno alipaswa kutambua kwamba tayari ana makosa na ana kadi moja hivyo ilimpasa kujilinda lakini akalisahau hilo na mwisho yakatokea yaliyotokea,” alisema Pluijm.

Kocha wa Simba, Mwingereza, Dylan Kerr, aliyekuwepo uwanjani hapo, naye alizungumza juu ya hilo: “Alichokifanya si kitendo cha kiuchezaji, amekuwa na hasira akashindwa kujizuia na akaigharimu timu na hasara ni kwa Yanga sasa, mchezaji hutakiwi kuwa hivyo halafu ukizingatia ni mtu muhimu, anapaswa kufuata falsafa za michezo uwanjani na kuisaidia timu yake na si vingine.”


Ngoma atakuwa nje ya uwanja kwenye mechi inayofuata dhidi ya Telecom ya Djibouti itakayopigwa keshokutwa Jumatano, kisha kurejea kwenye mechi dhidi ya KMKM ya Zanzibar.

Advertisement

 
Top