Gemu ya kwanza ya Simba msimu huu
itakuwa ni ile dhidi ya African Sport katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga
siku ya Jumamosi hii. Watacheza na JKT Mgambo siku tatu baadae katika
uwanja huo huo wa Mkwakwani.
UWANJA MGUMU KWAO…
Kwa misimu miwili iliyopita Simba
imeshindwa kupata ushindi katika mchezo wa kwanza wa msimu.
Walilazimisha sare ya 2-2 katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora
dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora ambayo ilikuwa ikicheza mchezo wake wa
kwanza wa ligi kuu msimu wa 2013/14.
Coastal Union ya Tanga ilitoka
nyuma kwa magoli 2-0 na kutengeneza sare ya 2-2 katika uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Simba msimu uliopita. Sasa
wanakwenda kuivaa timu ya African Sport ambayo itakuwa ikicheza mchezo
wa kwanza wa ligi kuu baada ya kusubiri kwa miaka 23.
Simba haijawahi kushinda katika
uwanja wa Mkwakwani katika gemu 6 zilizopita. Imetoa sare mara nne na
kupoteza michezo miwili. Sports wanaweza kuishinda Simba?. Wana kila
sababu ya kushinda, kupata matokeo ya sare lakini kupoteza itakuwa ni
sawa na mwanzo mbaya katika uwanja wa nyumbani mbele ya timu ambayo
haina rekodi ya kuvutia kwenye uwanja huo.
Sports haina wachezaji wenye
majina makubwa lakini wamejipanga vizuri kiutawala huku wakiwaongeza
wachezaji wazoefu kama Zahoro Pazzi, chini ya mwalimu Mlage Kabange timu
hiyo ya Tanga itaendeleza rekodi ya Simba kutoshinda Mkwakwani Stadium.
MECHI 6 BILA BAO MKWAKWANI, MGAMBO NI ‘NUKSI KWAO’…
Mechi ya pili ya msimu Simba
wataivaa JKT Mgambo ambayo katika misimu yake mitatu katika ligi kuu
haijawahi kupoteza dhidi ya Simba ndani ya uwanja wa Mkwakwani. Licha ya
kupoteza gemu zote walizowahi kucheza na Simba jijini Dar es Salaam
tena kwa idadi ya 6-0, 4-0, Mgambo imeichapa Simba mara mbili katika
gemu tatu za Tanga.
Walitoa suluhu-tasa msimu wa
2012/13, wakashinda 1-0 msimu wa 2013/14, wakashinda tena 2-0 msimu
uliopita. Mara zote hizo Simba haijafanikiwa kufunga goli. Pia timu hiyo
ya Dar es Salaam haijawahi kupata goli katika sare tatu mfululizo
walizopata dhidi ya timu nyingine ya mkoa wa Tanga ndani ya misimu
mitatu iliyopita.
MECHI YA KWANZA UWANJA WA TAIFA…
Kagera Sugar sasa ipo chini ya
mwalimu mshindi wa tuzo ya kocha bora wa ligi kuu bara msimu uliopita,
Mbwana Makatta. Timu hiyo ya Bukoba itacheza na Simba katika mchezo wa
mzunguko wa tatu ndani ya uwanja wa Taifa. Simba itakuwa ikicheza gemu
ya kwanza nyumbani msimu huu tena wakiwa wametoka katika uwanja mgumu wa
Mkwakwani, Tanga.
Inaweza kuonekana mechi rahisi
kwa kikosi cha Kerry lakini inaweza kuwa mechi ya kwanza ‘ngumu kuliko’
licha ya kwamba watakuwa katika uwanja wa nyumbani. Kushindwa kufunga
goli/magoli katika gemu dhidi ya Sports na Mgambo ni jambo ambalo
litaleta presha kwa timu hadi kwa mashabiki ‘wakereketwa’ wa klabu.
Kagera imefunga magoli manne
katika gemu mbili za mwisho dhidi ya Simba katika uwanja wa Taifa na
hawajapoteza mchezo wowote. Simba watakuwa na presha kwani gemu ya nne
ni dhidi ya mahasimu wao Yanga SC. Kabla ya kuwavaa Yanga watakuwa
wamekusanya pointi ngapi? Wanaweza kupata alama moja ama mbili katika
michezo miwili ya Tanga na Kagera wanaweza kuondoka na alama tatu au
moja katika mchezo wao wa mzunguko wa tatu.
