
Kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi (kushto) akiwa sambamba na kocha mkuu wa timu hiyo Hans van der Pluijm
Na Simon Chimbo
Msimu wa mwaka 2003-04 kocha
Mholanzi Martin Jol alikataa ofa ya kuwa msaidizi wa Sir Alex Ferguson
Manchester United na badala take kuendelea kuwa kocha mkuu wa klabu ya
RCK Waalwijk ya Uholanzi.
Baada ya kuondokewa na msaidizi
wake mreno Carlos Quiroz aliyehamia Real Madrid wakati huo, Martin Jol
alikataa ofa ya kumsaidia Ferguson Manchester United.
Hali kama hiyo imetokea nyumbani
Tanzania, ambapo baada ya kocha Charles Boniface Mkwasa kutakiwa na timu
ya taifa, klabu ya Yanga ikamhitaji Mwambusi kuwa msaidizi wao kuziba
nafasi iliyoachwa wazi na Mkwasa.
Tofauti na mholanzi Martin Jol,
kocha Juma Mwambusi hakupepesa macho kujiunga na Yanga kuwa msaidizi
hali akiacha nafasi ya ukocha mkuu wa Mbeya City.
Mjadala umekuwa ni mkubwa kwa
wadau wa michezo nchini wakijaribu kuhoji usahihi wa Mwambusi kuhusiana
na kuacha u-boss wa Mbeya City na kuwa msaidizi wa kocha mkuu wa Yanga.
Kuna kitu lazima tuwekane sawa
hapa; mfumo wa soka letu ni tofauti kabisa na soka la barani Ulaya.
Katika ligi yetu, na hali ilivyo halisi, hakuna uwiano kati ya vilabu
kongwe nchini vya Simba na Yanga na vilabu vingine, Azam pekee.
Tofauti ya kimfumo kati ya ligi
yetu na ligi zilizoendelea duniani ndiyo kitu kinachonifanya niamini
kuwa Mwambusi yuko sahihi kwa maana ya kwamba kalamba dume ama galasa.
Hakuna tofauti kubwa ya kimaslai,
wala fursa baina ya timu barani Ulaya na ndio maana klabu ndogo kamba
Wimbledon ina mashabiki wake na wanapata fursa sawa na klabu nyingine
yeyote.
Kwa Tanzania, tuende mbele turudi
nyuma bado ufalme wa klabu za Simba na Yanga katika soka letu ni mkubwa
sana. Ni ngumu sio tu kwa makocha, bali hata wachezaji kuzikatalia timu
hizo zinapowataka.
Ili uonekane na upate changamoto
na exposure ya kutosha kwa nchi yetu, lazima upitie Simba na Yanga,
achilia mbali Azam ambao hivi sasa wamekamilika na kuzifikia klabu hizo
ingawa bado linapokuja suala la ushabiki, bado Simba na Yanga ni wafalme
wa soka ya bongo.
Kiuhalisia, kutoka Mbeya City kwa
Mwambusi na kujiunga na Yanga ni hatua muhimu katika historia ya career
take ya soka. Mwambusi sasa atafahamika, ataongeza ujuzi na kupata
uzoefu wa kutosha kutokana na changamoto zilizopo katika klabu hizi
kubwa tofauti na Mbeya City.
Bila shaka fursa aliyoipata kocha
Boniface Mkwasa kuwa meneja wa timu ya taifa, imetokana na kiasi
kikubwa uwezo na uzoefu alioupata akiwa kocha msaidizi wa Yanga.
Kesho hatujui nini kiko mbele ya Mwambusi kama ambavyo hatukujua kilichokua mbele ya Mkwasa.
Ingawa sitaki kuzungumzia masuala
ya maslai ‘mtonyo’ ambao Mwambusi atanufaika zaidi akiwa Yanga tofauti
na ilivyokua City, lakini hicho pia sio kitu cha kubeza hasa kwa maisha
yetu ya kiswahili.
Profile ya Mwambusi sasa
imeongeza kitu na kwamba inampa mwanya wa kuwa na fursa nyingi kubwa
mbele yake kama ilivyomtokea Boniface Mkwasa ambaye sasa ni boss wa timu
ya soka ya taifa ya kandanda ya Tanzania.
Mwisho nitumie fursa hii kumtakia
kila la kheri mrithi was Mwambusi Mbeya City. Kuondoka kwa Mwambusi ni
fursa kwake na kwamba ni wakati wa yeye pia kutengeneza jina lake katika
ramani ya soka.