
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Licha ya kusisitiza kuwa straika
wake, Pape Ndaw ni mshambuliaji makini na mwenye uwezo mkubwa mkufunzi
mkuu wa Simba SC, Dylan Kerr atalazimika ‘kum-bust’ mshambuliaji na
nahodha wa timu hiyo Musa Hassan Mgosi ili kukabiliana na tatizo la
washambuliaji katika timu yake.
Simba ipo Mbeya tangu Jumatatu
hii kwa ajili ya gemu mbili dhidi ya Mbeya City FC siku ya Jumamosi na
Tanzania Prisons siku ya Jumatano ijayo katika uwanja wa Sokoine,
Mbeya.
Mganda na kinara wa ufungaji wa
timu hiyo Hamis Kiiza anasumbuliwa na majeraha, Daniel Lyanga itabidi
aendelee kusubiri hadi wakati wa usajili wa dirisha dogo na ili
kukabiliana na City, Kerr atalazimika kumtegemea zaidi Mgosi sambamba na
chipukizi, Ibrahim Ajib, Boniface Maganga na Msenegal, Ndaw.
“Ndaw ni mshambuliaji mwenye
vigezo, ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga pasi na kufunga”,
alikaririwa Kerr akimsifia mshambulizi huyo mrefu zaidi katika ligi kuu
Tanzania bara msimu huu.
Kiiza ametupia kambani magoli
matano kati ya 7 ya Simba katika gemu tano zilizopita, aliukosa mchezo
uliopita dhidi ya Kagera Sugar ambao Kerr alimpanga kiungo mchezeshaji
Peter Mwalyanzi katika idara ya mashambulizi sambamba na Ajib.
Faraja kubwa kwa Simba ni kurejea
katika kiwango kwa kiungo wao Jonas Mkude. Mechi hiyo inasubiriwa kwa
hamu na mashabiki wa kandanda nchini ambao wanataka kuona ni vipi City
itaanza maisha mapya bila mwalimu Juma Mwambusi aliyejiunga na Yanga.
Simba haijawahi kupata ushindi katika gemu nne zilizopita dhidi ya City
na mara ya mwisho walipokutana ‘Wekundu wa Msimbazi’ walilazwa 2-0.
Simba imeshinda gemu nne,
imepoteza mechi moja na ipo nafasi ya 3 ya msimamo ikiwa na alama 12
sawa na Mtibwa Sugar lakini kikosi cha Kerr kina wastani mzuri wa magoli
ya kufunga na kufungwa kuliko Mtibwa. Simba imeruhusu nyavu zake
kutikiswa mara tatu na kufanya wawe na wastani wa magoli Manne ya
kufunga na kufungwa.