Hatimaye kocha mkuu wa klabu ya Yanga SC, Mbrazil, Marcio Maximo amempata mshambulizi ambaye anaweza kubeba majukumu yaliyoachwa wazi na Geilson Santos ‘ Jaja’ katika safu ya mashambulizi. Danny Mrwanda ambaye amefunga mabao manne katika michezo saba msimu huu akiwa na timu ya Polisi Morogoro amekubali kusaini mkataba wa mwaka mmoja na Yanga.
Mrwanda, 31 aliahirisha mpango wa kurudi nchini Vietnam na alikuwa mbioni kurudi kwa mara ya nne katika timu yake ya zamani, Simba SC lakini, Yanga ndiyo wamiliki halali wa mchezaji huyo baada ya kumalizana na Polisi Moro na Danny mwenyewe kukubali kufanya kazi klabuni hapo hadi Disemba mwaka ujao.
Mrwanda ni mshambulizi mzuri kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira, kukimbia katika nafasi, kufunga na kupiga pasi. Ingawa Danny ana udhaifu wake, hasa kuinama sana chini, Maximo anatambua anaweza kuifanya safu yake ya mashambulizi kuwa ya hatari na yenye kasi. Mrwanda, Mrisho Ngassa na Saimon Msuva inaweza kuwa safu kali zaidi ya mashambulizi ndani ya Yanga ikiongozwa na wachezaji wazawa.
Yanga kumsaini, Danny ni jambo ambalo halikutarajiwa, lakini kitu cha kupendeza ni mchezaji mwenyewe kukiri kuwa hilo ni jambo la bahati, na amekubali kukabiliana na changamoto mpya katika timu yake mpya.
Kama wachezaji hao watatu watalinda viwango vyao ambavyo katika siku za karibuni vimekuwa juu, Maximo anaweza kuwa amepata mtu sahihi ambaye anawea kumpatia majukumu mengi katika safu ya mbele. Licha ya kimo chake kidogo ( kama ilivyo kwa Ngassa na Msuva), Danny ni mchezaji mwenye nguvu ambaye anaweza kusimama kama mshambulizi huru. Hivyo ndivyo anavyopendelea Maximo na bila shaka usajili huo usio na ‘ mbwembwe’ utakuwa na faida kwa pande zote.
                                                    
Mrwanda amepata bahati, na sasa atakuwa ni mmoja wa wachezaji ambao wamepata kucheza klabu kubwa za Tanzania-nazungumzia, Simba na Yanga, pia ana uzoefu wa kucheza Kuwait na Vietnam hivyo hakuna shaka kuwa kujiunga kwake na Yanga ni sehemu ya kutimiza ndoto za mwanasoka mkubwa. Klabu kubwa ziko kwa ajili ya wachezaji wakubwa, mrwanda ni mchezaji ambaye anaweza kujibu kila wasiwasi wa watu wa yanga na kuwafungia mabao kama atapewa sapoti.
Jaja aliamua kutorudi nchibni kutokana na matatizo ya kifamilia, lakini presha ambazo mashabiki wa yanga huwa wanazitoa kwa wachezaji wao ( hasa wale wapya) huwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kiwango cha chini cha wachezaji wao. Mara ya mwisho aliposajiliwa na Simba, 2012, Mrwanda alikumbana na presha kubwa katika michezo ya kagame Cup na hivyo alijikuta akitemwa mara baada ya michuano hiyo kumalizika.
msuvaa
Aliitwa ‘ mzee’ na kila alipoharibu mpira alikuwa akizomewa na mashabiki wa klabu yake ambao walikuwa wakimshinikiza kocha, Milovan Curkovic kumtoa nje mchezaji huyo. Yanga wasije kufanya hivyo, wachezaji wenye uzoefu kama Danny ni muhimu sana kwa timu yenye malengo makubwa. Mtazame Mussa Hassan Mgosi na msaada wake katika timu ya Mtibwa, si Mussa tu hata Shaaban Nditti na sasa Henry Joseph ni muhimu sana na wanamsaidia kocha wao Mecky Mexime.
Maximo ameshafanya kazi na Mrwanda wakati akiinoa timu ya Taifa, Taifa Stars, anamjua vizuri Danny na anajua ni kitu gani anaweza kukipata kutoka kwa mchezaji huyo. Jerry Tegete, Hussein Javu, Ngassa, Hamis Kizza, Msuva na Mrwanda, unaitazama Yanga na kuona imebadilika sana na sas inakuja na sura za ‘ Ki-Tanzania katika safu ya mashambulizi’


Advertisement

 
Top