BEKI wa Simba, Hassan Kessy, amekuwa shujaa katika macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini kutokana na uamuzi wake wa kususia kuichezea Simba.
Kessy ameamua kuchukua uamuzi wa kujiondoa kambini na kurejea kwao Morogoro kwa kuwa viongozi wa Simba wameshindwa kutimiza ahadi yao ya kummalizia fedha zake.

Kessy alitakiwa kulipwa Sh milioni tano iliyobakia baada ya kuwa amepokea Sh milioni 15 za awali katika fedha za usajili.

Sifa kwenda kwa Kessy ni nyingi, kwamba amechukua uamuzi mzuri na sahihi huku wengi wakiwatupia lawama viongozi wa Simba kama wababaishaji kwa kuwa wameshindwa kutekeleza ahadi.

Kessy amelalama kutolipwa fedha, lakini hakutafutiwa hata nyumba aliyoahidiwa, hali iliyomfanya aishi kwa kutangatanga jijini Dar kwa kuwa hakuwa na makazi!

Hilo pia ni kati ya mambo ambayo wadau wengi wa soka wamekuwa wakiyapigia kelele, kwamba halikuwa sahihi na beki huyo ni shujaa kwa kuamua kujiondoa.

Nilipoamua kuanza kufuatilia mkasa mzima, niligundua meneja wa beki huyo, Athumani Shaaban ‘Tippo’ ndiye anatupiwa lawama kubwa na viongozi wa Simba, kwamba anahusika kumshawishi Kessy.

Kwanza nianze na viongozi hao, kwamba hawapaswi kumlaumu sana Tippo, kama meneja lazima awe upande wa Kessy kwa kuwa ni mchezaji wake. Angeonekana ni mwendawazimu kama angelalia upande wa Simba na kumuacha Kessy.

Hivyo, kama Kessy ataamua “ujinga” au “sahihi”, Tippo atabaki kuwa upande wa mchezaji wake na hawezi kuwa upande wa Simba.

Katika hili la kutimiza ahadi, bado naamini viongozi wa Simba wamebabaisha na ilikuwa haina ujanja kwao zaidi ya kupambana na kutimiza ahadi yao ya kumlipa kama walivyokuwa wameahidi. Inawezekana walichelewa, basi ilikuwa ni vizuri kuzungumza naye kila mara kumueleza kuhusiana na mambo kwenda vigumu.

Hakuna ubishi, kama wamechelewa, hawakusema lolote na hawakuonyesha kujutia hilo, basi wamebabaisha mambo na wanapaswa kujifunza kwa kuwa watu wanawaamini, basi waonyeshe wanapaswa kuaminiwa na wanaowaamini hawajakosea hata kidogo.

Nikirudi kwa Kessy, nataka kupishana na wengi sana wanaomuona beki huyo ni shujaa, kuwa amefichua uozo. Naona Kessy ndiye aliyebabaisha zaidi.

Fedha alizotakiwa kulipwa ni haki yake, lakini kwangu, naamini wakati mwingine kuna njia sahihi ya kudai kuliko kutanguliza mgomo ambao hujenga picha tofauti kwa mtu yeyote, mfano “unaabudu fedha”, “una tamaa”, “huna mapenzi hata kidogo na klabu” na mengine mengi.

Picha hiyo inayojengwa inaweza isiwe sahihi hata kidogo, lakini namna unavyodai pia inaweza kuwa tatizo kwa kuwa lazima tukubali Simba ni taasisi ambayo ina madeni kwa maana kwamba inadaiwa na kudai.

Jiulize, wachezaji wangapi wa Simba wanadai na wanaendelea kucheza na katika mechi dhidi ya Kagera Sugar waliyocheza na kushinda waliendelea kubaki na kuitumikia kwa moyo mmoja na nguvu zote hadi ikashinda kwa mabao 2-1?

Kessy amejiunga na Simba katika dirisha dogo, hajafikisha hata mwaka tangu ajiunge na Simba. Fedha anazodai ni za usajili kwa mkataba wa miaka miwili. Hadi sasa hajatumikia hata nusu mwaka lakini ameshalipwa asilimia zaidi ya 70 ya fedha zake za usajili.
Bado angeweza kumaliza hata msimu halafu baada ya hapo, angeweka msimamo kwamba asingeweza kutokea kwenye kikosi utakapoanza msimu hadi amaliziwe fedha zake kwanza lakini si sasa, yeye hajatumikia hata nusu msimu, anagoma.

Sasa Simba inapambana bila yeye, wakati huu ndiyo ilimhitaji na angeweza kuonyesha angalau kidogo anaweza kuipigania hata katika wakati mgumu. Kuna ubaya?

Bado narudi kwake, ile ishu kwamba alikosa hata pa kuishi kwa kuwa hakupewa nyumba! Viongozi wa Simba walikosea, hili lazima wakubali na waachane na ahadi za hisia au hewa, badala yake watekeleze yaliyo katika mkataba.

Lakini kwa Kessy inanishangaza! Alipokuwa Mtibwa Sugar, mshahara haukuzidi Sh 350,000. Sasa Simba analipwa Sh milioni 1.5, kweli anashindwa kutoa angalau Sh 300,000 akapanga chumba na sebule?

Sasa kwa mshahara huo, vipi anakubali kuishi maisha ya kutangatanga wakati inaonekana mshahara wake umeongezeka mara tano?

Bado nashangazwa naye kutoona umuhimu wa kuendelea kuishi kwa kujilipia wakati akisubiri Simba wamtafutie nyumba. Tena ingewezekana kufanya nao majadiliano.

Kabla ya kufikia uamuzi wa kugoma, alizungumza na viongozi wangapi wanaohusika na Simba na kuwaeleza hali yake ya kutokuwa na furaha kuhusiana na mshahara wake?
Kweli tunamuona Kessy shujaa kwa kugoma, lakini shujaa wa namna gani aliyeishi kwa kutangatanga huku akiwa na mshahara wa Sh milioni 1.5 kwa mwezi?

Wewe muajiriwa kama mimi, haujawahi kucheleweshewa malipo hata mara moja? Wewe unayefanya biashara, haujawahi kucheleweshewa malipo hata mara moja na wale wateja wako? Nikuulize, ulisusa hata mara moja? Mbona bado unaendelea hadi sasa na maisha yanakwenda!
Matatizo kokote yataendelea kumkuta Kessy kwa kuwa hata kule alikokuwa akilipwa Sh 300,000 pia waliwahi kumcheleweshea na alicheza hadi mambo yalipotulia.

Leo anasusa yeye. Swali, kama akishalipwa na siku akatokewa na tatizo, kweli Simba hawawezi kumsaidia nje ya mkataba wake kama binadamu?


Tukumbuke kuna ambao Kessy amewakuta wanaichezea Simba, hadi leo wanaendelea kuidai na wanaitumikia. Hivyo kazi kwa kuwa inahusisha binadamu, haiwezi kuukimbia ubinadamu. Iko haja wakati mwingine kuangalia njia sahihi ili kutatua matatizo yetu!

Advertisement

 
Top