Hatimaye Simba sasa imekuwa na uhakika wa kumbakiza kiungo wake mbunifu, Awadh Juma baada ya kukubaliana kumwongezea mkataba wa miezi 18.

Awadh, mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, amekuwa akikubalika kwa kocha wake, Dylan Kerr ambaye mara kadhaa amekuwa akikiri kumkubali mchezaji huyo kiasi cha kukiri kuwa ndiye anayesaidia kuunganisha safu ya kiungo na ushambuliaji kikosini kwake.

Awadh alisema kuwa alimalizana na viongozi wa timu hiyo jana Alhamisi kwa kukubaliana kuongeza mkataba wa muda huo, ada ya usajili na mambo mengine ndani ya mkataba na kwamba kilichobaki sasa ni makabidhiano kisha yeye amwage wino.

“Tumemalizana, tumeshaelewana juu ya kila kitu kwamba nitaongeza mwaka na nusu, dau la usajili na mambo mengine, kwa hiyo bado kusaini ambapo natarajia zoezi hilo litakamilika ndani ya siku mbili hizi kabla ya mechi yetu na Azam FC,” alisema Awadh anayefananishwa na mchezaji wa zamani wa Ureno, Maniche.

Advertisement

 
Top